04/11/2009 9.49.31


Msalaba ni kielelezo cha upendo, umoja na huruma ya Mungu kwa watu wake! Si chanzo cha chuki na uhasama!


|

Baraza la Maaskofu Katoliki Italia limesikitishwa sana na uamuzi wa Mahakama kuu ya Jumuiya ya Ulaya inayoshughulikia haki msingi za binadamu, kutoa amri ya kuondolewa kwa misalaba yote iliyotundikwa kwenye shule na taasisi za elimu, kama njia ya kuheshimu uhuru wa kidini.
Maaskofu wanasema, huu ni uamuzi ambao unapata chimbuko lake katika masuala ya kisiasa, kiasi cha kusahahu au kushindwa kutambua maana ya Msalaba kwamba si tu kielelezo cha kiimani bali pia unafumbata mwelekeo wa kitamaduni.
Uwepo wa Msalaba katika maeneo ya hadhara ni mang'amuzi na utambuzi wa mchango wa misingi ya kikatoliki na urithi wa wananchi wa Italia, kama inavyobainishwa kwenye Makubaliano ya Mwaka 1984. Maaskofu wanasema, uamuzi huu wa mahakama unataka kutenganisha kimsingi utambulisho wa kitaifa, misingi ya maisha ya kiroho na kitamaduni. Hali hii inaweza kuzua kinzani na migongano isiyokuwa ya lazima.
Padre Federico Lombardi, Msemaji mkuu wa Vatican anabainisha kwamba, kimsingi Msalaba ni kielelezo cha upendo wa Mungu, umoja na mshikamano kati ya watu. Inasikitisha kusikia kwamba, Msalaba sasa unakuwa ni kielelezo cha kinzani, migawanyiko na ukosefu wa uhuru. Mawazo kama haya ni kinyume kabisa na uelewa wa wananchi wa Italia.
Ni jambo lisilokubalika kuondoa katika mazingira ya elimu, kielelezo cha tunu msingi za kidini, katika historia na utamaduni wa watu wa Italia. Dini inachangia kwa kiasi kikubwa katika majiundo na makuzi ya mwanadamu kimaadili, na kielelezo makini cha utamaduni na maendeleo ya mtu. Ni kosa la kiufundi na mwono finyu kabisa kung'oa Msalaba katika maeneo ya majiundo ya watu.
Padre Federico Lombardi anasema, kitendo hiki kinasikitisha na kutia uchungu, kwani mwelekeo wa sasa ni kutotaka kutambua mchango wa Kikristo katika majiundo ya watu wa Ulaya, ukweli ambao kamwe hautaweza kupindishwa.
|