04/11/2009 10.52.52


Taalilimungu ya moyo ikuze majadiliano na taalilimungu akili, ili kuondokana na kiburi cha kisomi katika mafumbo ya imani


|

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, siku ya jumatano, tarehe 4 Oktoba, 2009 aliendelea na katekesi yake, akifanya ulinganisho wa kitaalimungu kati ya Mtakatifu Bernard Clairvaux na Mtakatifu Abelard, wote ni wasomi wanaongaliwa katika mwelekeo wa imani inayotafuta kufahamu zaidi. Baba Mtakatifu anasema, mahali ambapo Mtakatifu Bernard alipenda kukazia zaidi kuhusu imani, Mtakatifu Abelard akaweka msisitizo kwenye uelewa.
Taalimungu mintarafu Mtakatifu Bernard ilipania kumwezesha mwamini kuwa na mang'amuzi ya Mungu dhidi ya kiburi cha kisomi, kinachowafanya baadhi ya watu kudhani kwamba, wanaweza kuyafahamu mambo yote yanayojikita katika Fumbo la Imani.
Mtakatifu Abelard alipania zaidi kutumia mang'amuzi ya kifalsafa katika taalimungu na hatimaye, kung'amua kutoka katika dini za watu wengine ile mbegu inayowafunulia uelewa wa Kristo. Maelekeo haya mawili anasema Baba Mtakatifu kati ya watakatifu Bernard na Abelard; taalimungu ya moyo na taalimungu ya akili yalizua kinzani.
Yote haya yanabainisha umuhimu wa majadiliano ya kina katika medani ya kitaalimungu na utii kwa viongozi wa Kanisa. Taalimungu haina budi kuheshimu misingi iliyopokelewa kutoka katika Ufunuo inapoendelea kuipatia tafsiri sahihi kadiri ya mwanga wa kifalsafa.
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita anasema, kunapotokea kinzani za kitaalimungu, kila mtu, lakini kwa namna ya pekee, viongozi wa Kanisa wanao wajibu wa kulinda na kuhifadhi imani katika ukamilifu wake. Baba Mtakatifu anawaombea waamini wanapoendelea kujifunza Injili, Mwenyezi Mungu aweze kuwaimarisha katika ukweli na upendo.
Baba Mtakatifu akizungumza na waamini pamoja na mahujaji kwa lugha mbali mbali amewaasa kuwa waaminifu kwa imani iliyofunuliwa kwa Mama Kanisa pamoja na kujitahidi kuwa ni wahudumu wa ukweli na upendo kwa moyo na akili zote.
Baba Mtakatifu akizungumza na waamini kutoka Poland alimkumbuka Mtakatifu Karoli Borromeo, ambaye Mama Kanisa anafanya kumbu kumbu yake tarehe 4 Novemba, kila mwaka kwa kuelekeza mawazo yake kwa Hayati Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa pili.
Mfano wa maisha na mafundisho yake yawaimarishe waamini katika imani pamoja na kuwapatia changamoto ya kuchuchumilia utakatifu wa maisha. Amekazia pia moyo wa sala unaojikita katika nyimbo za kidini, kama njia ya kushehenesha mioyo kwa imani na matumaini, ili hatimaye, kutolea ushuhuda wa imani, kwa kutangaza matendo makuu ya Mungu katika maisha.
|