05/11/2009 8.58.34


Mshikamano wa dhati, mafao ya kizazi kijacho na mabadiliko ya mtindo wa maisha; ni mambo ya kuzingatiwa katika agenda ya nishati


|

Askofu mkuu Celestino Migliore, Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa anasema, teknolojia rafiki inayoheshimu na kutunza mazingira, mapambano dhidi ya umaskini, ushirikiano wa kimataifa unaojengeka katika misingi na kanuni ya auni, ubadilishanaji wa taarifa na teknolojia ni kati ya mambo ambayo yanaweza kusaidia Jumuiya ya Kimataifa kulinda na kutunza mazingira.
Askofu mkuu Migliore anasema, Nchi Changa duniani zinauwezo wa kudhibiti uchafuzi wa mazingira ikiwa kama zitawezeshwa kwa njia ya mtaji na teknolojia, ili kutumia umeme wa jua na ule unaozalishwa kutokana na maporomoko ya maji, bila kusahau uwezekano wa kuwa na matumizi ya nishati uoto. Mwelekeo huu utaziwezesha nchi changa duniani kukabiliana kwa kiasi kikubwa na ongezeko la mahitaji ya nishati pamoja na kujiletea maendeleo endelevu.
Majadiliano kuhusu nishati hayana budi pia kuangalia madhara yanayoweza kuwapata binadamu na uharibifu wa mazingira kwa siku za baadaye. Busara na umakini katika maamuzi ya kimataifa kwani madhara ya uchafuzi wa mazingira ni matokeo ya nchi zilizoendelea duniani, lakini nchi maskini zinaathirika pia kutokana na maamuzi haya bila kusahahu changamoto za mabadiliko ya tabianchi.
Askofu mkuu Celestino Migliore anasema, matumizi ya teknolojia rafiki ni changamoto kuanzia kwa mtu binafsi, sekta binafsi na serikali katika ujumla wake. Matumizi ya nishati yazingatie pia haki kwani, kizazi kijacho kinaweza kuonja pia madhara ya matumizi tenge ya nishati duniani, hali ambayo inahitaji Jumuiya ya Kimataifa kubadili mtindo wa maisha yake, kwa kukazia kanuni ya mshikamano unaovuka mipaka ya kitaifa na kiuchumi.
Matumizi ya nishati inapaswa kuwa pia ni agenda katika masuala ya kielimu, ili kuwawezesha wananchii kuwa na sera nzuri katika maendeleo ya nishati na matumizi yake kama njia ya kudhibiti mabadiliko ya tabianchi na madhara yake katika jamii.
|