06/11/2009 9.49.01


Hati ya kichungaji kwa watumiaji wa barabara, watoto wanaoishi katika mazingira magumu pamoja na wanawake


|

Baraza la Kipapa la shughuli za kichungaji kwa ajili ya wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum, limetoa hati itakayosaidia juhudi za Mama Kanisa katika utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu kwa watumiaji wa barabara. Hati hii ni matokeo ya mkutano wa wawakilishi kutoka Bara la Ulaya uliofanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 29 Septemba hadi 2 Oktoba, 2009 hapa mjini Vatican.
Hati hii inalenga kuwahudumia watumiaji wa barabara na reli; kuwakomboa na kuwapatia uhuru wa kweli wanawake na wasichana wanaojikuta wakitumbukizwa kwenye biashara ya ngono barabarani pamoja na kuweka mikakati makini, ili kuwasaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu na wale wasiokuwa na makazi.
Hati inapembua na hatimaye kutoa mapendekezo ambayo yanapaswa kufanyiwa kazi, ili kulinda na kudumisha utu na heshima ya mwanadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Utume wa kichungaji kwa watumiaji wa barabara ni kielelezo cha ushuhuda wa kiinjili, waamini wakikumbushwa kwamba, kimsingi, Injili ilianza kuhubiriwa barabarani na sasa, Mama Kanisa anataka kuwahubiria kwa mara nyingine tena katika mazingira tofauti watumiaji wa barabara.
Lengo ni kuwawezesha watu hawa kuweza kukutana na Kristo, kila mtu kwa namna yake binafsi, ili hatimaye kupata wongofu wa ndani, utakaopelekea na wao kuendelea kutolea ushuhuda wa Injili katika mazingira yao. Kuna watu wanateseka na kutaabika njiani, kumbe hija ya imani linakuwa ni jambo linalohitaji Uinjilishaji wa kina, ingawa mara nyingi watu wamekuwa na woga.
Jitihada za Mama Kanisa kuweka mikakati ya kichungaji kwa ajili ya watumiaji wa Barabara na reli, ni kuwasindikiza katika hija ya maisha na shughuli zao, kwa kutambua na kuthamini mchango na dhamana wanayobeba kwa abiria na mizigo yao, lakini pia ni wasi wasi wa Mama Kanisa kutokana na kuongezeka kwa ajali na uharibifu wa mali na miundo mbinu kutokana na matumizi mabaya ya vyombo vya usafiri.
Ajali na vifo vimeongezeka maradufu, hali inayokwenda sambamba pia na ongezeko la vyombo vya usafiri, ikilinganishwa na miaka kadhaa iliyopita. Lakini, uchu wa kupata faida kubwa, kubana matumizi ya muda na gharama, hofu ya kupoteza nafasi ya ajira ni mambo yanayowafanya madreva kuwa na msongo wa mawazo, kiasi cha kusababisha ajali za mara kwa mara ambazo kimsingi zingeweza kudhibitiwa.
Madreva hawa wamekuwa wakiendesha magari kwa masafa marefu, wakiwa mbali na nyumbani pamoja na familia zao, hali ambayo inawafanya kukosa ule mwingiliano wa kijamii. Matokeo yake, baadhi yao wanajikuta wakitumia vilevi na dawa haramu za kulevya. Mama Kanisa anatambua na kuthamini mchango wa watu wanaofanya kazi katika sekta ya usafirshaji, wanatiwa shime kuendelea kujikita zaidi katika maadili, kanuni na matumizi bora ya njia za mawasiliano, wakiheshimu zawadi ya maisha.
Wafanyakazi hawa wanahitaji kuoneshwa moyo wa mshikamano, ili kuwatia ari na nguvu katika shughuli zao, ili kupambana na upweke hasi unaoweza kupelekea hata kujisikia kwamba wanatengwa na jamii. Mshikamano huu unahitajika hasa zaidi kwa wale wanaofanya shughuli zao nyakati za usiku.
Baraza la Kipapa la shughuli za kichungaji kwa wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum, linaweka mikakati kwa ajili ya kuwasaidia wanawake wanaojikuta wakitumikishwa kwenye biashara ya ngono; wengine hufariki dunia wakiwa bado njiani. Kuna sababu nyingi zinazopelekea watu kuzikimbia au kuzihama nchi zao, hii ikiwa ni pamoja na mawazo finyu. Yote haya wakati mwingine yanawatumbukiza watu hata kwenye biashara haramu ya binadamu.
Biashara ya wanawake Barani Ulaya inashamiri kwa sababu wanatumiwa katika biashara ya ngono au kwa ajili ya kazi za nyumbani. Itakumbukwa kwamba, hata wanaume na watoto wanajikuta pia wakitumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu. Yote haya yanapelekea watu hao kuathirika kwa dawa za kulevya, kupata magonjwa hasa Ukimwi pamoja na kukosa makazi bora hali inayotendea utu na heshima yao kama binadamu.
Bishara haramu ya binadamu inafanyika pia ndani kwa ndani, yaani wanawake wanasafirishwa kutoka sehemu moja ya nchi kwenda sehemu nyingine kwa ajili ya biashara ya ngono na huduma za majumbani. Zote hizi ni dalili za umaskini miongoni mwa watu. Mama Kanisa anapenda kuchukua fursa hii kusaidia jitihada za Jumuiya ya Kimataifa kuzuia uhamiaji haramu, kwa kutoa taarifa makini, usalama na hatari wanazoweza kukumbana nazo, watu wanapoamua kuhamia Ulaya.
Mfumo dume pia ni chanzo cha biashara haramu ya binadamu pamoja na ngono. Kuna haja ya kudumisha mtandao utakaosaidia kupambana fika na biashara haramu ya binadamu na ukahaba kwa Kanisa kushirikiana na Serikali pamoja na asasi za kiraia. Lakini, ikumbukwe kwamba, Kanisa linaendelea kutekeleza dhamana hii kwa njia ya mashirika ya kitawa pamoja na kuwaonesha mshikamano kwa kuishi nao huko waliko.
Shughuli za kichungaji kwa ajili ya watoto wanaoishi katika mazingira magumu zinapaswa kupewa kipaumbele, kwani hatya ni matokeo ya kubomoka kwa misingi na tunu bora za kifamilia, hali inayowafanya watoto hao kukosa malezi na huduma msingi katika maisha yao kiasi cha kuwageuza kuwa ni omba omba mitaani. Mama Kanisa anapenda kuwafikia watoto hawa mahali walipo, ili kuweza kuwasaidia kwa hali na mali.
Lengo ni kuweza kuwarejesha tenda ndani ya familia zao, jambo linalohitaji maandalizi kamambe na watu walioandaliwa kwa kazi hii. Kanisa linawaalika waamini na watu wenye mapenzi mema kuwajengea watoto wanaoishi katika mazingira magumu mwelekeo chanya na matumaini kwa siku za usoni badala ya kuwabebesha shutuma za uvinjifu wa sheria na matendo yote yanayokwenda kinyume cha utu na heshima ya binadamu.
Kanisa linapenda kuwa ni sauti ya kinabii kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu, ili kusimama kidete kulinda na kutetea haki zao msingi kwa kuzingatia mazingira, tamaduni na imani ya watoto husika. Sheria za nchi husika zinaweza kusaidia kupata haki msingi za watoto wanaoishi katika mazingira magumu; kwa kukazia upendo na hatimaye kuwajengea mazingira yatakayowasaidia kuanzisha uhusiano wa kirafiki pamoja na kuwaamini wale wanaowahudumia.
Mashirika mengi ya kitawa yameendelea kuwa ni msaada mkubwa kwa ajili ya kuwasaidia na kuwahudumia watoto wanaoishi katika mazingira magumu. Kwa njia ya mfumo wa elimu, Kanisa linaweza kusaidia jitihada za kupambana na tatizo la watoto wanaoishi katika mazingira magumu, kwa njia ya kuwawezesha katika elimu ili kupambana na mazingira yao.
Utamaduni na imani ya watu ni mambo ya kuzingatiwa wakati wa kutoa huduma kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu. Kanisa linapenda kuendelea kushirikiana na Serikali hasa kwa ajili ya kuwahudumia maskini, katika mikakati yake ya kichungaji.
Shughguli za kichungaji kwa ajili ya watu wasiokuwa na makazi ni changamoto ya kupambana na umaskini. Kanisa linaweza kutekeleza dhamana hii kwa kutenga sehemu ya rasilimali yake pamoja na kushrikiana na wadau mbali mbali katika mapambano dhidi ya umaskini, kwa kuhakikisha kwamba, watu wanashirikishwa kikamilifu kwa ajili ya maendeleo yao endelevu; kwa njia ya upendo kwa jirani. Serikali kwa upande wake inajali zaidi usalama na ulinzi wa kijamii.
Utu na heshima ya mwanadamu havina budi kupewa kipaumbele pamoja na kudumisha urafiki mwema na watu wasiokuwa na makazi kwa kuzingatia mahitaji ya mtu mzima kiroho na kimwili. Watu wasiokuwa na makazi wasaidiwe kwa huduma mbali mbali ili kukidhi mahitaji yao msingi kwa kuweka mikakati ya muda mfupi na mrefu.
Kuna sababu kadhaa zinazowafanya watu kujikuta hawana makazi na hivyo kulazimika kulala barabarani. Hawa wasichukuliwe kama mzigo kwa jamii, bali waonjeshwe upendo na uvumilivu, kwa kuwasikiliza na kuwajali katika shida na mahangaiko yao. Waamini wanakumbushwa kwamba, watu hawa ni changamoto pia katika maisha yao. MAPENDEKEZO YANAYOTOLEWA
Kuna haja kwa Kanisa Barani Ulaya kuwa na mwamko mpana zaidi, utakaoliwezesha kuanzisha mikakati ya kichungaji kwa watumiaji wa njia za mawasiliano. Familia na shule ziwe ni mahali pa majiundo endelevu pamoja na kuheshimu imani na tamaduni za watu. Ateuliwe mhusika maalum kutoka katika Mabaraza ya Maaskofu Katoliki atakayekuwa na dhamana ya kuwasaidia watumiaji wa njia za mawasiliano. Watu wapewe habari ya kutosha kuhusu usalama wao.
Kutokana na kuongezeka kwa vitendo vya kigaidi, ajali barabarani na majanga asilia kuna haja ya kuwepo na watu maalum watakaotoa huduma wakati wote. Lakini, washauri wa kiroho na watu wa kujitolea wanapaswa kuandaliwa barabara sanjari na kushirikiana na watu wa kutoka sekta nyingine kama vile ya afya. Wadau mbali mbali washirikiane kutoa katekesi pamoja na kanuni za usalama barabarani, hali inayopaswa kwenda sambamba na jitihada za upatanisho na majadiliano ya kidini na kiekukeme.
Mama Kanisa awe pia mstari wa mbele kulinda na kutetea haki msingi za watumiaji wa barabara. Shughuli za kiparokia ziguse pia wale wanaotumia barabara katika maeneo ya Parokia husika. Kanisa lijiwekee utaratibu wa kukutana na watumiaji wa barabara katika maeneo maalum pamoja na matumizi ya radio zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa.
Mwongozo wa matumzi ya barabara uliotolewa na Baraza hili la kipapa unapaswa kusambazwa, ili kuokoa maisha na mali za watu. Kanisa kwa upande wake, likuze na kukazia mwelekeo wa kifamilia ili kuwasaidia watumiaji wa barabara na familia zao kuweza kuungana.
Jitihada za kuwakomboa wanawake kutoka katika biashara haramu ya ngono, lazima zizingatie: historia na upekee wa kila mtu, kwa kujenga na kukuza uhusiano mwema utakaomfanya mtu yule kujiaminisha kwa wahusika. Shughuli za kichungaji zihusishe masuala ya kijamii, kitamaduni na kidini. Mama Kanisa anaweza kutekeleza utume wake kwa kukazia uhusiano, maisha ya kisakramenti na huduma za kiroho.
Wanawake waliokolewa kutoka katika utumwa mamboleo wakaribishwe na kushirikishwa katika maisha ya Kanisa mahalia, kama sehemu ya mwendelezo wa kazi ya ukombozi. Wadau katika shughuli hizi za kichungaji, pale inapowezekana wapatie mafunzo maalum na kitaaluma ili kuifanya kazi hii kwa ufanisi zaidi. Makleri na watawa katika majiundo yao wawezeshwe kupata elimu itakayowasaidia katika shughuli zao za kichungaji.
Utu na heshima ya wanawake iheshimiwe na kuthaminiwa na wadau mbali mbali na kwamba, mwili wa mwanadamu ni hekalua la Fumbo la Utatu Mtakatifu na wala si nyumba ya biashara. Watu waelimishwe wajibu na haki zao msingi katika maisha kwa kushirikiana na taasisi za elimu katika ngazi mbali mbali za maisha. Tatizo la biashara haramu ya binadamu halina budi kupewa msukumo wa pekee kwa kukazia majadiliano ya kitamaduni, ili kulinda na kudumisha utu na heshima ya wahanga wa biashara hii.
Jitihada hizi za uponyaji wa ndani ziwasaidie wanawake hao kujisikia kuwa wanathaminiwa na kupendwa, ili kuwapatia mwelekeo mpya katika maisha, mabadiliko haya yaguse pia wadau wanaotoa huduma kwa wanawake hawa. Watu wanaofanya utume wao katika mazingira magumu hawana budi kufikiriwa kwani wanaweza pia wakati mwingine kuhatarisha maisha yao. Shughuli za kichungaji zipambanue na kubainisha maeneo husika, pale inapowezekana ushirikiano uwepo ili kuwa na matumizi mazuri zaidi ya rasilimali
USHAURI WA KICHUNGAJI KWA WATOTO WANAOISHI KATIKA MAZINGIRA MAGUMU.
Mama Kanisa anapaswa kuwa ni sauti ya kinabii kwa watoto wanaoishi katika mazingita hatarishi kwa kusaidia kutunga sheria na kanuni zitakazosaidia kudumisha majadiliano ya kina katika ngazi mbali mbali. Shughuli hizi ziwe ni sehemu ya mikakati ya kawaida ndani ya parokia husika, kwa kuzisaidia kuimarisha misingi ya familia zilizovunjika, ili kuangalia uwezekano wa kuwarudisha watoto hao ndani ya familia zao asilia.
Wazazi na walezi wanaalikwa kuwa ni mifano bora ya kuigwa na pale inapowezekana familia zijitolee kuwachukua na kuwalea watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi; kwa kusaidia kutoa elimu na majiundo endelevu pamoja na upatanisho. Mikakati iwekwe ili kuzuia kubomoka kwa misingi na tunu bora za maisha ya kifamilia, kwa kutambua na kuthamini haki za watoto ili ziweze kuheshimiwa na kuthaminiwa ndani ya Jamii.
Mama Kanisa anapewa changamoto ya kuanzisha shughuli za michezo ili kutoa mwanya kwa watoto na vijana kupata mahali pa kukutania. Baraza la Kipapa linapendekeza majiundo makini kwa wahudumu wa Injili. MAPENDEKEZO YA KICHUNGAJI KWA WATU WASIOKUWA NA MAKAZI
Mama Kanisa anapewa changamoto ya kuwa ni kielelezo cha ukarimu na upendo katika huduma zake za kichungaji, kwa kuwawezesha watu, ili waweze kuwajibika, kushiriki pamoja na kujiunga tena ndani ya jamii, hali inayowataka wahudumu wa Injili kujiendeleza katika masuala ya kiufundi, kisaikolojia na katika maisha ya kiroho. Watu wasiokuwa na makazi waonje ukarimu huu kutoka katika Parokia kwa kutoa nafasi kwa watu hao, sanjari na mapambano dhidi ya umaskini.
Inashauriwa kwamba, mashirika yanayojihusisha na watu wasiokuwa na makazi yanapaswa kuwa na utawala makini na miundo mbinu , ili kutekeleza utume wao kwa kuwa na mwelekeo na tunu ambazo wanataka kuzishirikisha katika maisha ya kijamii. Kanisa liendelee daima kuwa ni sauti ya kinabii kwa kukazia tunu za kiutu na zile za kiinjili.
Watu wasiokuwa na makazi wanapaswa kuhudumiwa katika parokia wanamoishi pamoja na kushirikishwa katika maisha na utume wa Mama Kanisa, sanjari na kupata huduma ya ibada ya mazishi kama ni wakristo pamoja na kukumbukwa katika sala na sadaka. Kanisa halina budi kuanzisha mtandao utakaoratibu shughuli kwa ajili ya watu wasiokuwa na makazi pamoja na kuwahabarisha watu ili waweze kufahamu ukubwa wa tatizo lenyewe.
|